NDEGE WA AJABU

SEHEMU YA ISHIRINI-20

“Anaua bila huruma, anakula mioyo ya wanadamu haijalishi mwanadamu aliye hai au aliye fariki. Binti. Sarai wewe utulivu wako ndio utakao kuponya, yamkini ukafanikiwa kurudi nyumbani kwenu salama kuliko ukiendelea kuleta papara ndani ya msitu huu wenye kila aina ya mnyama. Usione upo tulivu ukajua uko salama, la hasha humu ndani kuna balaa, kuna fujo za wanyama. Nipo hapa nitakusaidia ingawa, kinacho takiwa sasa ni wewe kuniamini mimi kuliko kuleta hofu juu yangu, kumbuka imani yako ndiyo itakayo kuponya binti na si vinginevyo, papara itakupeleka pabaya” Alisema Ajuza yule, maneno hayo alikuwa akimwambia Fatma binti ambaye alitaka kuondoka ndani ya himaya ya kikongwe huyo aishie msituni peke yake. Hapo ndipo Fatma alipo ogopa, hadithi ya kuhusu maisha ya msitu ule yalimfanya atulize munkari aliyo kuwa nayo. Lakini licha ya kupunguza munkari, alipata wazo kichwani mwake, nalo ni kumwambia ajuza yule amrudishe nyumbani kwao kama ataweza. Ila baadaye wazo hilo akalifutilia mbali, aliona ni upuuzi kwa kuwa ajuza hatoweza kumrudisha nyumbani kwao. Wala hata hakujua kama Ajuza yule sio kiumbe cha kawaida, ni Ajuza wa ajabu kabisa. Ana kila aina ya balaa, ni yule yule bibi kizee aliye nusurika kuuliwa na Chifu Gato siku ile aliyo mtupia maneno ya shombo juu ya kuuliwa kikatili mjukuu wake. Pasipo kutegemea Gato  Bibi kizee yule alipotea mbele ya macho yake kwa kupigwa na radi, na huo ndio ukawa mwanzo mwisho wa kikongwe yule kuonekana kijijini Lundu, ngome ya Chifu katiri wa kuitwa Gato. Kidume cha mbegu, jitu lenye milaba minne, sura mbaya yenye makovu makovu kama paja la changudoa mazoefu asiye ogopa halaiki ya watu.  Kiganja chake kigumu mithili ya mkono wa nyani mwenda peke, mdomo wake nao muda wote mkavu ilihali akitema mate machafu kana kwamba udongo. Chifu Gato.

“Hebu kunywa dawa hii itarudisha nguvu na hali mpya iliyo potea kwa muda” Ajuza alisema. Fatma akashusha pumzi ndefu kwanza akatulia na kisha kunywa dawa ile aliyo kuwa akipewa anywe. Alikunywa kwa kugugumia, ilikuwa chachu kama maji ya limao, hata hivyo alikunywa funda la kwanza na la pili tu halafu Ajuza akakiweka kando kibuyu kile kidogo alicho tumia kama kikombe. Sasa akageuka kutazama moto ule kwenye mafiga, ajabu miale miwili myembamba mithili ya shoti ya umeme ikatokea kwenye mboni za macho yake na kisha kugonga kwenye kiota kile cha moto, ghafla moto ukaongezeka. Akatabasmu akageuka kumtazama Fatma nyuma yake, naye akamuona akiachia tabasamu murua huku akiwa amejikunyata ingawa poleni pole aliajiachia, na hiyo ikawa ishara tosha kuwa anahisi joto badala ya baridi kama ilivyo kuwa hapo awali.

Igwene baada msoto mkubwa, hatimaye kijana huyo machachari anafanikiwa kuliona pango lile alilo mhifadhi Fatma. Aliachia tabasamu bashasha kamwe hakuamini kama kweli amefanikiwa kuliona pango hilo, alilitafuta sana ni baada tu kuwakimbia Askari wale wa Chifu Gato, sasa juhudi zake zinazaa matunda, pasipo kutarajia anajikuta ameliona pango lile. Hakika ikawa furaha upande wake, kiu yake sasa ikawa ni kutaka kumuona Fatma ambaye mara ya mwisho alimuacha akiwa na njaa kali.

Kabla hajaingia ndani ya lile pango, alitazama kwanza kila upande. Alipo jihakikishia usalama ndipo akaingia huku akimuita kwa sauti ya chini iliyo jaa shauku.

“Sarai..Sarai.. Sarai. Nimerejea samahani kwa kuchelewa. Sarai itika tafadhali itika nimerudi Igwene” Alipaza sauti yake Igwene kumuita Fatma. Hakujua kama binti huyo amesha chukuliwa na Ajuza wa ajabu aishie ndani ya msitu huo.

Hakukata tamaa aliendelea kumuita huku akizama ndani zaidi ya pango lile, lakini mwishowe akagundua kwamba Fatma hayupo mule ndani. Ghafla akachachawa, akatoka ndani haraka sana wakati huo akijiuliza wapi alipo elekea binti huyo aliye kula naye nadhiri ya kutoroka  himaya ya Chifu Gato. Alipo fika nje ya pango alipaza sauti kwa mara nyingine tena kumuita Fatma. Sauti yake ikasambaa eneo kubwa la msitu. Hatimaye Bullah anaisikia, alisimama ili kuisikiliza kwa umakini, nia yake ikiwa ni kutaka kujua wapi inapo tokea sauti ile. Hatimaye akajua, haraka sana akawahamasisha wenzake wamfuate, aliongoza njia walionekana kukimbia mbio za kasi mithili ya Nungunungu, nia yake ilikuwa ni kumkamata Igwene na pia kumpata Sarai kisha kurejea nao kwenye Ngome. Wakati Bullah na wenzake wakimfauata Igwene, kijana huyo naye aliketi chini huku akiendelea kulia kwa uchungu, aliwaza wapi atakapo mpata Fatma ambaye yeye alimfahamu kwa jina Sarai, jina ambalo binti yule alipewa na Chifu Gato.

Kilio chake mwisho kilikoma, ni baada kuhisi mwili ukimsisimka. Dalili hiyo ilimshtua sana akahisi kuna kitu kisicho cha kawaida kina mnyemelea. Upesi alisimama akatazama huku na kule,, ndivyo hali ile ilivyo zidi kuongezeka mwilini mwake. Mwishowe akakata kauli ambapo aliona heri atoweke mahala hapo kwa haraka sana iwezekanavyo aende kutulia sehemu nyingine kisha apange mkakati wa kumsaka Fatma. Dhumuni lake lilokuwa moja tu ambalo ni kutoweka naye kama walivyo kubaliana hapo awali. Hatua kadhaa alizo piga kutoka pale lilipo pango, ghafla akasikia kishindo kikubwa nyuma yake. Akageuka kutazama nyuma, hapo alipata kuona kiumbe kisicho eleweka kuwa ni kiumbe cha aina gani kikiishia ndani ya lile pango.

“Mmh! Ni nini kile?” Alijiuliza ndani ya nafsi yake Igwene, alitamani kikiona usoni kiumbe kile ili atambue ni kiumbe cha aina gani, si hivyo tu bali alihisi kwamba huenda pango lile ndiyo makazi ya kiumbe kile,

“Au ndiye yule ndege wa ajabu aliye semwa sana miaka kwa miaka?” Igwene aliongeza kuwaza.

“Hebu ngoja nijifiche hapa, yani leo mpaka nijue ukweli. Lazima nikione kiumbe hiki” Alikata kauli, akaona heri ajifiche, kiu yake ni kutaka kuona kiumbe kile kilicho ingia pangoni. Kwa miaka mingi iliyo pita tangu akingali mdogo amekuwa akisikia hadithi kadha wa kadha kuhusu ndege wa ajabu inavyo semekana ndege huyo karne kwa karne.

Mithili ya maji ya mtungini ndivyo Igwene alivyo tulia kwenye kichaka kile ambacho kilimficha vizuri, macho yake akayaelekezea kule pangoni alionekana kuwa makini haswa. Lakini wakati subira ya kutaka kumuona yule kiumbe ambaye hakumtambua ikiwa imetanda moyoni mwake, mara ghafla pale nje ya pango alionekana moja ya Askari wa Chifu Gato. Askari yule alikuwa akitazama huku na kule, punde akainama na kuinuka. Kwenye kiganja chake alikuwa ameshika mkufu ambao aliutazama kwa umakini, akaugeuza geuza kwa taharuki kubwa ilihali muda huo huo Igwene akatazama kifua chake akagundua kuwa mkufu ule ambao awali alitoka nao pangoni umeacha pale nje ya pango sasa umechukuliwa na yule Askari wa Chifu Gato.

Lakini yule Askari baada kuutazama kwa kina mwishowe akaurudisha pale pale, alitaka kuingia ndani ya pango lile ila hofu ikamjaa ambapo ilipelekea kuogopa, na hivyo basi akapiga mrunzi kuwaita wenzake. Punde si punde Bullah alifika mahala hapo akiwa na askari wengine.

“Nahisi Igwene atakuwa ndani humo” Alisema Bullah. Akang’ata tunda poli alilokuwa akilila, alimeng’enya akameza kisha akamgusa bega yule Askari walio mkuta mahala pale.

“Wewe ingia ndani ukamuangalie na sisi tunafuata nyuma” Aliongeza kusema.

“Mimi?” Askari yule alihoji kwa sauti ya woga iliyo jaa wasi wasi tele, ukweli wa mambo pango lile lilikuwa linatisha sana.

“Mmh! Ndio wewe unatakiwa uingie humo ndani, mimi ndiye nimekuteua kama kiongozi wako. Lazima ufuate kile nikisenacho” Bullah alijibu kwa sauti ya kujiamini huku akiwa amekunja sura yake.

“Aah lakini kiongozi…”

“Nyamanza kimya mbwa wewe!” Kabla Askari yule hajasema alicho taka kusema, ghafla Bullah akadakia na kisha kumwambia maneno hayo kwa jazba sanjari na kuchomoa kisu kwenye kara.

“Sikiliza! Nimesha pinda mpaka muda huu! Naweza kukutoa utumbo sasa hivi endapo kama utaendelea kuwa mbishi” Aliongeza kusema Bullah huku akimtishia kisu Askari mwenzake. Songombingo hilo lote ambalo lilikuwa likiendelea, kijana Igwene alikuwa akilishuhudia pale kichakani, balaa lingine hilo upande wake. Utulivu zaidi ulichukua nafasi kwani Askari hao wanamtafuta yeye, hivyo endapo kama watajua yuko mahala hapo, basi hawato ingia pangoni bali watakula naye sahani moja. Na wakati Igwene yupo mahala hapo akiuendeleza utulivu, punde akahisi ubaridi kwenye mguu wake, alipo shusha macho kutazama sehemu hiyo akapata kuona nyoka mkubwa akimtambaa pole pole kuelekea kwenye nyeti zake.

JE, NI KIPI KILICHO ENDELEA?.. DAVID AMEFARIKI? NA VIPI KUHUSU YULE KIUMBE ALIYE INGIA PANGONI? NDIYE NDEGE WA AJABU? HAYO NA MENGINE MENGI TUKUKUTANE EPISODE INAYO FUATA ILI KUJUA UKWELI WA MAMBO.

Leave a comment

Design a site like this with WordPress.com
Get started